UJENZI WA RELI YA KISASA UTALETA NAFUU KWA WASAFIRI
Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kujenga reli ya
kisasa. Reli hiyo itaanzia Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kigoma na Mwanza.
Abiria wanaosafiri kwenda mikoa hiyo watakuwa wakitumia saa nane kufika mwisho
wa safari. Reli hiyo itakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Mwanza na
Kigoma na mikoa mingine ya jirani.
Kwa mfano abiria waliokuwa wakisafiri kwenda mikoa ya Kigoma
na Mwanza,kwa treni ya kawaida walikuwa wanatumia siku tatu safarini. Treni
zilizokuwa zikiondoka Dar es Salaam siku ya Jumapili jioni saa 11.00 zimekuwa
zikifika mkoani Mwanza na Dar es Salaam siku ya Jumanne. Kwa ujumla safari hizo
zimekuwa ni za kuchosha.
Lakini tatizo jingine ambalo limekuwa ni kero kubwa kwa
abiria wa treni, ni kuharibika kwa vichwa vyake kutokana na kuchakaa. Jingine
ni kusombwa kwa reli hususan wakati wa mvua,hususan mkoani Morogoro.
Kwa vyovyote iwavyo usafiri wa treni umekuwa ni wa bei nafuu
kwa watu wa vipato vya chini kuumudu. Hata kwa sasa ambapo abiria wengi
wamekuwa wakihangaika kwa usafiri wakati wa misimu ya sikukuu za Krismas na
mwaka mpya, reli za kuelekea mikoa ya Kaskazini zitawaletea ukombozi mkubwa.
Haitakuwa rahishi kupandishiwa bei na wamiliki wenye mabasi. Wataweza kusafiri
kwa faraja. Tuombe serikali ifanikishe lengo hilo.