
Shirika lisilo la kiserikali la Twaweza lilitoa taarifa ya
hali ya rushwa hapa nchini.Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze
alieleza kuwa viwango vya rushwa vimepungua kwa mwaka 2017 ukilinganisha na mwaka
2014.Hata hivyo taasisi mbili za serikali zilikuwa bado zinaongoza kwa vitendo
vya rushwa.Taasisi hizo ni Jeshi la Polisi na Mahakama. Kwa mfano kwa mwaka
2014, vitendo vya rushwa vilifikia asilimia 60 lakini vikashuka kwa asilimia 39
kwa mwaka 2017.
Ingawaje tatizo la rushwa haliwezi kuisha kabisa, walio wengi waliyapokea matokeo ya utafiti
huo ulioonesha kupungua kuwa ni
kiashiria kizuri cha ushindi wa mapambano dhidi ya rushwa. Zipo jitihada
zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kudhibiti kuenea kwa rushwa na
matumizi mabaya ya madaraka. Kuna kesi zilizofunguliwa mahakamani.Baadhi ya
watuhumiwa wamehukumiwa na kutumikia vifungo gerezani. Wanaoendelea kupokea ama
rushwa bila shaka wanajua kikamilifu kuwa siku zao zinahesabiwa.
Pamoja na utafiti huo kubainisha rushwa kupungua, kulikuwa
na mawazo ya watu waliohojiwa wakieleza mapambano dhidi ya rushwa yanadidimiza
kukua kwa uchumi.Mawazo kama hayo yalikuwa ni
ya kushitua ndani ya fikra za watu wanaopambana na vitendo vya rushwa. Ilikuwa
ni tafsiri ambayo haina maelezo ya kuridhisha kwani uchumi unaathirika vipi
katika mapambano hayo wakati wananchi wanaporwa haki zao? Je, mawazo ya namna
hiyo yanawakilishwa na kundi gani? Ni kundi la walionacho ama wasionacho? Ni
dhahiri hayo yalikuwa ni mawazo ya walionacho..
Kwa mfano uchumi unaathirika vipi ikiwa wananchi wamekuwa
wakilazimishwa na watumishi wa serikali kulipia huduma ambazo wangezipata bure?
Kwa utawala wa awamu ya tano ambapo wananchi wanasifia huduma zimeimarika, Je,
si ndiyo uchumi unaimarika zaidi kwani imani yao kwa serikali imeongezeka. Miaka michache
iliyopita, wananchi walikuwa wamepoteza imani kwa serikali yao jambo ambalo lilikuwa ni hatari kwa sifa
na uchumi wa taifa letu.
Ilikuwa imefikia hatua ambapo wananchi wa kawaida walikuwa
wanajiona kuwa wao si chochote wala lolote mbele ya watumishi wa umma. Nao
watumishi wa umma wakawa wanajiona kuwa mabwana wa kuwafanyia watakavyo
wananchi wa kawaida.Tunaisikia kauli mbiu ya Rais Dk. John Pombe Magufuli
akiweka waziwazi kuwa serikali yake itawatumikia wanyonge. Kauli hiyo inatolewa
na kiongozi huyo kwa kufahamu kile kilichokuwa kikiwapata wananchi wa kawaida
walipokuwa wakitaka huduma kutoka kwa watumishi wa umma.
Mojawapo kati ya maamuzi ambayo yanakubaliana na kauli hiyo
ni kuwaruhusu wachimbaji wadogowadogo wa madini kufanya shughuli zao bila
kubughudhiwa. Ukiutafakari uamuzi huo, unaweza kugundua kuwa kulikuwa na
viashiria vya rushwa vilivyokuwa vikiwapendelea wachimbaji wa madini wa
makampuni makubwa.Kufuatia hali hiyo, tulikuwa tukisikia jinsi wachimbaji wa
madini wadogowadogo walivyokuwa wakipigwa
virungu na Polisi,kuumizwa na hata kuuawa wakiwatetea wachimbaji wa
makampuni makubwa. Wao ndiyo walikuwa na
haki zaidi ya watanzania wazalendo.
Na uamuzi huo ni dhahiri kwamba Dk. Magufuli anaamini endapo
wachimbaji hao wanaporuhusiwa wataisaidia serikali katika kulipa kodi na hivyo
kuongeza pato la serikali.
Dk. John Pombe Magufuli
alikuwa hajaridhishwa na jinsi Kampuni kubwa za kuchimba madini
zilivyokuwa zinalipa kodi. Hilo
liliweza kuthibitishwa pale makontena ya mchanga wenye dhahabu yalipokamatwa
kwenye bandari ya Dar es Salaam.Kampuni ya Barrick Gold Corporation
ilipojitokeza kukiri kuwa mmiliki wa makontena hayo, ilibainika ilikuwa
ikikwepa kulipa mamilioni ya kodi. Kwa namna yoyote hatuwezi kukana ukweli
kwamba huo ulikuwa ni mmojawapo wa mikakati wa kupambana na vitendo vya rushwa.
Tumesikia kuwa baada ya kukiri kukwepa kulipa kodi hiyo, sasa Kampuni ya
Barrick Gold Corporation imekubali kuilipa serikali ya Tanzania kiasi cha shilingi bilioni
700. Ni dhahiri fedha hizo zitasaidia katika kuwaletea wananchi maendeleo
yanayotakiwa. Kama serikali isingesimama
imara, fedha hizo zingewanufaisha watu wa mataifa ya nje na kuwaacha watanzania
katika umaskini.Watanzania wote kwa ujumla wanapaswa kushiriki kikamilifu
katika mapambano dhidi ya rushwa. Ikiwezekana rushwa itokomezwe kabisa.