Monday, January 08, 2018

WASAFIRI WA MWEZI DESEMBA WATAFARIJIWA NA KUKAMILIKA KWA TRENI YA KISASA





WASAFIRI WA MWEZI DESEMBA  WATAFARIJIWA NA KUKAMILIKA KWA TRENI YA KISASA


Kila unapofika mwezi Desemba kila mwaka,watu wengi hushawishika kusafiri kuliko miezi mingine  yoyote.Sikukuu za Krismas na mwaka mpya, zinatoa msukumo kwa watu kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Wengi hupendelea sikukuu hizo ziwakute ama  ziwaunganishe na familia zao. Katika hali ya kawaida, mwezi wa Desemba umekuwa  na ongezeko la ajali nyingi za barabarani. Magari huwa yanabeba abiria wengi kupita kiasi na wakati huohuo madereva wa magari ya abiria kuzembea kuzingatia kanuni za usalama barabarani. Askari wa usalama barabarani wanakuwa na kazi kubwa ya kukagua na kuhakikisha madereva wa magari ya abiria wanaendesha kwa makini ili kuepusha ajali.

Ni katika kipindi cha mwezi huu wa Desemba, ambapo nauli za mabasi ya  abiria huongezeka maradufu. Baadhi ya wamiliki wa mabasi ya abiria hukitumia kipindi cha mwezi wa Desemba, kujitafutia faida kubwa kwani wanafahamu watu wengi wanapenda kusafiri. Ni katika mwezi huu wa Desemba vitendo vya udanganyifu na utapeli huwa vinaibuka na kuwasababishia hasara abiria.

Kusafiri kila unapofika mwezi Desemba ni vizuri, kwani siyo hapa Tanzania tu bali  hata huko Ulaya idadi ya wasafiri huongezeka. Tofauti inayojitokeza huku kwetu, ni uchache wa mabasi ya abiria yanayotosheleza mahitaji yao. Kwa kadri ya safari za mwezi Desemba abiria wengi wamekuwa wakilazimika kulala kwenye vituo vya mabasi, wengine kujazana na kukosa viti vya kukalia na kugeuka kuwa kero na taabu kwao.

Katika kukabiliana na ongezeko kubwa la wasafiri kwa mwezi Desemba, wakati uliopita serikali ilikuwa ikilazimika kutoa vibali kwa taasisi ama Kampuni nyingine kusafirisha abiria. Ninakumbuka Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) kiliwahi kushiriki kusafirisha abiria katika msimu wa mwezi Desemba. Hata kwa sasa kama serikali inaweza kutoa maamuzi kama hayo mapema, itasaidia kuwapa faraja wasafiri kuondokana na kero zinazojitokeza mwezi Desemba.

Lakini lililo bora zaidi katika kuleta faraja kwa watanzania, ni pale ujenzi wa reli ya kati ya kisasa kutoka Dar es Salaam kuelekea Kigoma na Mwanza, na ile inayoelekea mikoa ya Kaskazini itakapokuwa imekamilika. Abiria wataweza kusafiri kwa Gari Moshi Unafuu wake unatokana na ukweli kwamba nauli zake zitakuwa nafuu ukilinganisha na nauli zinazotozwa na mabasi ya abiria.

Usafiri kwa Gari Moshi ni salama zaidi. Hakuna tishio la kuvamiwa na majambazi kama ilivyo kwa usafiri wa magari ya abiria ambao huvizia kutafuta fedha.Usafiri kwa Gari Moshi utaisaidia serikali kuokoa maisha ya watanzania wengi wanaofariki kutokana na ajali  zinazotokea mara nyingi mwezi wa Desemba.

Kwa sasa hivi ni kama vile abiria wenye vipato vya kawaida, wanalazimika kusafiri kwa mabasi.Lakini pale reli hizo zitakapokuwa zimekamilika zitawawezesha abiria kupanga na kuchagua aina ya usafiri wanaoupenda. Ni ukweli unaokubalika kwamba wengi wanapenda kusafiri mwezi Desemba kwa sababu  zilizojadiliwa kwenye makala hii,wakati mwingine inakuwa ni kero kubwa kwa kufikiria matatizo ya usafiri yakiwemo ajali ama wizi.Serikali kwa dhamira yake ya kujenga reli ya kisasa, iharakishe kuikamilisha na itakuwa neema kwa watanzania watakaokuwa wakisafiri kila unapofika mwezi Desemba.Watakuwa na fursa ya kupanga bila hofu safari zao.