Serikali ya Tanzania imeamua kwa dhati kabisa kupiga mnada
maelfu ya ng’ombe wote
wanaoingizwa nchini kinyume cha sheria kutoka kwa nchi
majirani.Nchi majirani wa Tanzania ambao ng’ombe wao wamekuwa wakiingizwa
nchini kwa kisingizio cha kutafuta malisho ni Kenya, Uganda na Rwanda.
Alipokuwa kwenye
ziara ya kikazi mkoani Kagera,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John
Pombe Magufuli alisisitiza msimamo huo. Magufuli anasema kwa kuwa Tanzania
inafanya hivyo, vivyo hivyo na nchi majirani wa Tanzania wawapige mnada ng’ombe
watakaokuwa wameingizwa kinyume cha sheria kutoka nchini Tanzania.
Licha ya
Kenya,Uganda na Rwanda kuwa majirani, lakini pia ni wanachama wa Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki. Matamshi ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kuhusiana na
uingizwaji wa mifugo, yaliwashitua baadhi ya watu.lngawaje tayari kiasi cha
ng’ombe zaidi ya 1000 kutoka nchini Kenya walikuwa wamepigwa mnada.Yalikuwepo
malalamiko kutoka kwa waliodai kuwa walikuwa wamiliki wa ng’ombe kutoka nchini
Kenya, lakini serikali ilisema waliopigwa mnada hawakuwa na mmiliki wake.
Katika mahusiano ya ujirani mwema, kulikuwa na matumaini
kwamba serikali ya Tanzania ingeweza kuwaonea huruma wafugaji wanaoingiza nchini ng’ombe wao kinyume cha sheria.
Kulikuwa na madai kwamba serikali ya Tanzania imefanya makosa makubwa kiasi cha
kuhatarisha ushirikiano wa mataifa hayo ya Afrika ya Mashariki.Msimamo wa
serikali ya Tanzania unazidi kusisitiza kwamba hakuna ushirikiano katika uhalifu.
Kwa maana hiyo wafugaji kutoka nchi majirani wanaoingiza mifugo yao kinyume cha
sheria wanapaswa kushughulikiwa kama wahalifu wengine.
Tanzania inayo ardhi kubwa. Inatoa ushawishi kwa nchi
majirani kudhani kwamba wafugaji wanaweza kuvuka mipaka na kufanya watakavyo
kwa kisingizio cha ushirikiano uliopo miongoni mwa mataifa hayo,kumbe sivyo.Tanzania
inastahili kuzionya nchi majirani kwa kutoa adhabu kali dhidi ya wafugaji
wakorofi. Hapa hapa nchini tatizo la wingi wa mifugo bado ni tatizo linalosababisha
athari mbalimbali miongoni mwa wakulima na Wafugaji. Kumekuwa na matukio ya
wafugaji na wakulima kupigana, kujeruhiana hadi kuuana. Maisha mengi ya
watanzania yamekuwa yakipotea kutokana na wingi wa mifugo.
Mwanzoni ilidhaniwa serikali ya Tanzania inakabiliana na
tatizo la mifugo ya watanzania, kumbe
ndani yake wamo wafugaji kutoka nchi za Rwanda,Uganda na Kenya.Fikiria ni mzigo
kiasi gani unaobebwa na serikali ya
Tanzania kwenye suala hilo? Ni haki kweli serikali inyamaze eti kwa kuhofia
kuvuruga uhusiano na majirani zake? Siyo hivyo tu, baadhi ya watanzania
walikuwa wanafanya biashara ya kutunza mifugo ya wafugaji kutoka nchi majirani.
Yako matumaini makubwa kwamba baada ya serikali ya Tanzania
kutoa msimamo huo kwa kutoa adhabu kali, migogoro ya muda mrefu ambayo imekuwa
ikiwanyima amani watanzania kuhusiana na mifugo itakuwa imepata
ufumbuzi.Mwanzoni ilidhaniwa ni tatizo la ndani kumbe hata majirani zetu
wamekuwa wakichangia katika kuleta matatizo ya majeruhi na maafa. Amani na utulivu hapa nchini
iliyodumishwa kwa muda mrefu na viongozi waliopigania uhuru, ilikuwa
ikiharibiwa kwa ushirika wa nchi majirani.
Kama ambavyo serikali imekuwa haina huruma dhidi ya watu,
kikundi ama taasisi kinachokusudia kuvuruga amani ya watanzania ni wakati
sahihi kutofanya mzaha wa kuchezewa na wafugaji kutoka mataifa ya nje.
Wafugaji wanaoingiza mifugo kinyume cha sheria kutoka nchi
jirani, wanapaswa waadhibiwe kikamilifu kwa kujulishwa wanachokifanya ni sawa
na kuchezea amani, usalama na utulivu hapa nchini.Imekuwa siyo siri kwamba
katika uingizwaji wa mifugo, makundi ya uhalifu mbalimbali yamekuwa yakijificha
kama vile majangili hata majambazi.
Sekta ya Utalii
imekuwa ikiathirika kutokana na wanyama wanaowashawishi watalii kuja nchini
kupungua ama kutoweka kabisa. Zipo taarifa za kupungua kwa idadi ya Tembo na
hata wanyama wengine. Ni bora kabisa kwa serikali ya Tanzania kudhibiti na
kukomesha kwa kutoa adhabu kali wafugaji kutoka nchi za majirani kwa faida ya
amani na utulivu wa taifa letu.