Je, unadhani binadamu anapougua kwa muda mrefu anayo haki ya kuomba aharakishiwe kufa mapema?Maisha ya binadamu ni zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu. Hakuna uhalali kwa mtu yeyote kukatisha uhai wa mtu. Lakini baadhi ya nchi zimetoa ruhusa kwa mgonjwa aliyeugua kwa muda mrefu, kutoa idhini kwa madaktari wanaomuuguza mgonjwa kuruhusu afe mapema.Ruhusa hiyo inatia simanzi na majonzi kwa mgonjwa anapotoa ruhusa hiyo.
Uthubutu wa kuruhusu mgonjwa(mtu) ajifie mapema au haraka inatajwa kwa neno la kiingereza liitwalo'euthanasia'. Tafsiri yake inatajwa ikimaanisha kuwa ni kitendo cha kukatisha maisha ya mgonjwa ambaye inaelekea hawezi kupona, ama ni mzee.
Euthanasia inaweza kufanywa kwa aina mbalimbali. Kwa hatua ya kwanza,mgonjwa anaweza kuridhia ajifie mapema. Aina nyingine inaweza kufanyika pasipo kumhusisha mgonjwa aliye mahututi.Kwa vyovyote iwavyo,uthubutu wa kukatisha maisha ya mtu ambaye ni mgonjwa, haukubaliki kwani ni wa kujichukulia madaraka ya mwenyezi Mungu ambavyo sivyo.
Katika imani ya kikristo,mgonjwa anapokuwa mahututi huombewa kwa mwenyezi Mungu ili mapenzi yake amuepushe na kifo.Lau kama siyo hivyo basi kama akimchukua, ampokee katika ufalme wake.
Nchini Tanzania kumekuwa na matukio ya watu kujinyonga. Baadhi wamekuwa wakifanya hivyo kutokana na wivu wa kimapenzi, kushindwa mitihani, madeni sugu na mengineyo mengi. Maamuzi hayo yamekuwa yakichukuliwa kama suluhisho la kilichowakuta. Vitabu vitakatifu vya mwenyezi Mungu, vinakataza wanadamu kuchukua maamuzi ya kukatisha maisha yao. Vinawaelekeza kazi hiyo wamuchie mwenyezi Mungu pekee. Mathalani kwenye Biblia kitendo hicho kinatajwa kuwa ni dhambi.
Kwenye biblia hiyohiyo, inasema kwa kuifanya dhambi hiyo kutakuwa na swali la kujibu kwaa nini binadamu alichukua uamuzi huo
Kwa sheria za Tanzania, ni kosa kwa mtu kukatisha maisha yake. Ndiyo maana endapo mtu aliyekusudia kukatisha maisha yake akishindwa kufanikisha lengo hilo, anashitakiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria
Katika utamaduni wa kiafrika inatambulika kuwa kifo ni lazima. Lakini katika hali ya kawaida kulazimisha kufa ni uamuzi unaowashitua wengi. Kifo kipo na kinapotokea kwenye familia kinasababisha ;pengo Kuna watu waliokuwa wakimtegemea marehemu, ambao baadaye huathirika.
Matukio ya watu kukatisha maisha kwa kujinyonga, kunywa sumu ama mengineyo yamekuwaa yakitajwa kuwa yanaweza kupata suluhu. Wanasaikolojia wanasema ushauri nasaha ni muhimu kwa watu wanaoonesha kukata tamaa ama dhamira ya kukatisha maisha yao mapema. Lakini vile vile kuwa na subira ni muhimu ili kuepukana na janga hilo