Monday, January 08, 2018

TUSIIPOKONYE MADARAKA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI(NEC) TANZANIA KUWAIGA MAJIRANI



Mahakama ya juu nchini Kenya ilimtangaza Uhuru Kenyata kuwa Rais nchini humo.
Uamuzi huo unatokana na kesi mbili zilizokuwa zimefunguliwa kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika mara mbili, wa kwanza ukiwa uliofanyika mwezi Agosti mwaka huu. Katika uchaguzi huo uliofanyika mwezi Agosti, Uhuru  Kenyata alitangazwa kuwa mshindi. Tume huru ya Uchaguzi  na Mipaka chini ya Mwenyekiti(IEBC) Wafula Chebukati alidaiwa kuvuruga uchaguzi huo.

Raila Odinga mpinzani wa Uhuru Kenyata alikuwa na matarajio makubwa ya kupata haki yake kupitia Mahakama hiyo. Kwa mfano pale Jaji David Maraga alipobatilisha matokeo ya uchaguzi wa marudio , vyama vya upinzani vilidhani uchaguzi huo ungeweza kurudiwa tena na kuruhusu kuundwa kwa serikali ya mpito.Wafuasi wa Raila Odinga hawakufurahishwa na maamuzi hayo ilhali wale wa Uhuru Kenyata walikuwa wakiyafurahia.

Ngome kubwa ya upinzani ya Raila Odinga bado iko katika mji wa Kisumu,ambako katika uchaguzi wa hivi karibuni ulisusiwa. Kuna wafuasi wengi wa Odinga kule Mombasa na sehemu ya mji wa Nairobi.Wote hao bado wanaendeleza upinzani dhidi ya utawala  wa Uhuru Kenyata.

Wakati ambapo kwa sasa kwa kiasi fulani hali ya kisiasa ni shwari. Rais mteule Uhuru Kenyata anatarajiwa kuapishwa kuitawala nchi ya Kenya. Wakati Jaji Mkuu David Maraga alipofuta matokeo ya uchaguzi wa mwezi Agosti,watu wengi walisifia maamuzi hayo.
Kwa mfano hapa nchini Tanzania wapinzani waliisifia katiba ya Kenya inayoruhusu matokeo ya uchaguzi kupingwa mahakamani. Inaeleweka hapa nchini Tanzania kwamba matokeo ya uchaguzi, hususan wa Rais hayawezi kutenguliwa baada ya kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC)

Kuna athari ambazo ziliweza kujitokeza nchini Kenya kufuatia taratibu za kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais kupitia Mahakamani, ambazo ni kudidimia kwa shughuli za kiuchumi.Lakini vile vile ni gharama kubwa za kusimamia na kuendesha uchaguzi ambazo ni kama vile zinapotea bure. Fedha hizo zingeweza kutumika katika kuendeleza shughuli za maendeleo.

Nchini Tanzania katiba tuliyonayo ambayo inaipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi( NEC) kuwa ndiyo yenye madaraka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa kiti cha urais, imesaidia kukabiliana na madhara yatokanayo na utaratibu wa kupinga matokeo kupitia Mahakamani. Kitu chema kilichozingatiwa kwenye  Katiba ya Tanzania , ni kupunguza gharama za kurudia uchaguzi. Katika hukumu iliyotolewa nchini Kenya na kisha kumtangaza Uhuru Kenyata kuwa Rais, utagundua ni sawa na kile kilichofanywa na Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)kwamba ingawaje ililaumiwa kwa kuvuruga uchaguzi huo, ni kama vile Mahakama ya juu imekubaliana nayo. Kwa tafsiri nyingine inaweza kuelezwa kwamba Mahakama hiyo ilikuwa inajaribu kuwapa matumaini wapinzani, kumbe sivyo.

Tulielezwa kuwa wakati Jaji Mkuu David Maraga alipofuta matokeo ya uchaguzi wa mwezi Agosti, jaji mmoja miongoni mwa waliosikiliza rufaa ya wapinzani alitofautiana na wenzake. Jaji huyo hakukubaliana na sababu za kutengua matokeo ya kura za uchaguzi uliompa ushindi Uhuru Kenyata. Sasa kama wakati ule Mahakama hiyo ilipinga, iweje wapinzani hoja zao hazikusikilizwa?

Baadhi ya mapendekezo ya wapinzani kuwa ingeundwa serikali ya mseto inayounganisha pande zote, ama kurudia uchaguzi huo hayakuzingatiwa na Mahakama hiyo.Huku watu wengi  wakiwa wamejeruhiwa na kuuawa nchini Kenya, wananchi wanaendelea kutoridhishwa na ushindi wa serikali iliyoko madarakani.

Kwa kuzingatia kile kilichojitokeza nchini Kenya, kwa watanzania inabidi tukubaliane kuwa hata kama haki ya wapiga kura inaweza kupatikana Mahakamani ni maamuzi magumu sana kufuta na kuruhusu uchaguzi urudiwe.Kwa hekima ya hali ya juu kabisa, kuiachia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania kuwa ndiyo yenye madaraka ya mwisho kuhusiana na uchaguzi, ni suluhisho la kuepusha migogoro,kupoteza muda wa wapiga kura na gharama za uchaguzi.

Kwa kadri ya matakwa ya vyama vya upinzani na wanaharakati wengineo, kutaka kuwe na Tume huru ya uchaguzi kuliko iliyopo kwa sasa ni sahihi kimaandishi.Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza ikajumuisha kifungu kinachoruhusu wagombea kupinga matokeo ya urais Mahakamani, lakini kwa uzoefu haitakuwa rahisi maamuzi ya Mahakama kutofautiana na matokeo yaliyotangazwa na kuthibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC)

Ni vizuri wanaharakati na viongozi wa vyama vya upinzani wakajikumbusha kwamba hata pale Jaji David Maraga alipotoa hukumu hiyo, walio wengi walitoa maoni yao wakisema ilikuwa ni ya aina yake na nadra sana. Siyo kwamba majaji wa mataifa mengine hawakuweza kutoa hukumu kama hiyo, bali kwa upande mwingine wanazingatia athari za kiuchumi na za uchaguzi kwa mataifa yao.

Kwa hapa Tanzania kwa mazingira yetu, bado Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) inafaa kuthibitisha na kutangaza kura za viongozi bora wanaokubalika kwa watanzania na hata wale wa mataifa ya nje. Ingekuwa kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya Tanzania inawapitisha marais ambao ni hatari kwa usalama na mshikamano wa watanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi( NEC) ingekuwa ni muhimu isiwe na madaraka iliyonayo.

Na kwa vyovyote iwavyo, hata kama wapiga kura watapewa haki ya kwenda Mahakamani ama Tume ya Taifa(NEC) kuwa na madaraka, haitawezekana maamuzi yake yakawafurahisha wote kwa wakati mmoja.Watanzania wayakubali matokeo ya uchaguzi kwa kuwa baada ya miaka mitano,maamuzi mengine yanaweza kufanyika.


Imekuwa siyo ajabu kwa mfano hapa Tanzania, kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge zimekuwa zikichukua muda mrefu kufikia  hata zaidi ya miaka miwili. Kwa ulinganifu huo, kipi kinachofaa kama siyo kusubiri hadi ifike miaka mitano na kuchagua mbunge mwingine anayekubalika? Watanzania  waikubali na waiamini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)