Wednesday, May 23, 2018

RASILIMALI ZA MAJI KAMA VILE SAMAKI NI MUHIMU WALINDWE



  Nchini Tanzania kumekuwa na uvuvi haramu wa Samaki. Uvuvi huo haramu umekuwa ukifanyika kwa kutumia nyavu zisizofaa, kutumia mabomu na hata kutumia sumu. Hali hiyo imekuwa ikisababisha madhara kwa samaki wachanga na hatimaye viumbe hao kupungua kwa kasi.

     Katika kuhakikisha viumbe hao wanalindwa, serikali iliamua kuanzisha operesheni maalum kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu. Lakini hata kabla ya kuanzishwa kwa operesheni hiyo, tayari serikali ilikuwa imetoa elimu kwa wavuvi wote ili wajiepushe na uvuvi haramu.

Kwa kuwa operesheni hiyo imefanyika nchi nzima, nyavu za wavuvi ambazo haziruhusiwi katika uvuvi huo zilichomwa moto ama kuteketezwa kabisa. Kwa kiasi kikubwa idadi ya wavuvi ambao walikuwa wakijihusisha na uvuvi haramu, mali zao zimeharibiwa.

Katika kikao cha Bunge la Bajeti linaloendelea huko mkoani Dodoma, wabunge wameonesha kutoridhishwa na jinsi operesheni hiyo ilivyofanyika. Wamelalamika kwamba wavuvi wamenyanyaswa na maofisa wa serikali waliokuwa wakisimamia zoezi hilo.

Kutokana na kutoridhishwa na mwenendo huo, wabunge hao walitoa mapendekezo ya kutaka iundwe tume ya kuchunguza ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa operesheni hiyo.

Kwa ujumla wake, wabunge hao walikuwa na haki yao ya kikatiba kukosoa utaratibu huo. Hata hivyo ulinzi wa rasilimali za majini ni muhimu sana kwani kwa muda mrefu uvuvi huo haramu umekuwa ukifanyika. Ni wakati kwa wavuvi wakubali kufuata maelekezo ya serikali. Walipewa muda wa kutosha waache. Walaji wa Samaki wanataka walishwe samaki wanaofaa kwa afya zao