Jeshi la Ulinzi la Zimbabwe wiki hii lilitangaza kutwaa
utawala wa taifa hilo, lakini lilikana kufanya mapinduzi ya kumuondoa
madarakani Rais Robert Mugabe. Rais Mugabe alizuiliwa asitoke nyumbani kwake,
lakini jana (Ijumaa) aliweza kuhudhuria sherehe za mahafali ya chuo kikuu huria
mjini Harare na kutunuku shahada kwa wahitimu mbalimbali.
Kumekuwa na majadiliano kati yake na wanajeshi wanaoongozwa
na mkuu wa Jeshi la Zimbabwe Costantine Chiwenga,wakishinikiza Mugabe atangaze
kustaafu u rais wa nchi hiyo na
kumuachia Makamu wake,Emmerson ‘Mamba Mnangagwa anayekubalika kwa wanachama wa
Chama tawala cha ZANU-PF na wanajeshi. Na wakati huo huo, viongozi wa mataifa
ya nchi za Jumuiya ya maendeleo kwa nchi za kusini mwa Afrika(SADC) nao wanakutana
kujadili namna ya kupata suluhisho la mgogoro ulioko huko Zimbabwe.
Hata hivyo msimamo wa viongozi wa SADC ni kuhakikisha kwamba
mgogoro huo unatanzuliwa kwa kuzingatia katiba ya nchi hiyo. Mwenyekiti wa
Umoja wa Afrika Alpha Conde naye hali kadhalika aliungana na msimamo wa
viongozi wa SADC. Alikilaani vikali kitendo kilichofanywa na Jeshi la Zimbabwe
na kusema kamwe hakitambui wala kuunga mkono.
Viongozi wa mataifa ya Ulaya kama vile Uingereza, Ujerumani
ama Marekani ambayo kwa wakati uliopita yalikuwa yakimtaja Robert Mugabe kama
kiongozi ‘dikteta’, yameutaka mgogoro huo umalizwe kwa majadiliano na kwa
kufuata katiba ya nchi.
Robert Mugabe uhusiano wake na mataifa ya Ulaya ulitetereka
kutokana sera yake aliyoifanya ya kutaifisha mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa
na wazungu na kisha kuwagawia wazimbabwe.
Kulikuwepo na ukosoaji mwingi uliokuwa ukipinga maamuzi
mazito ya Robert Mugabe kwamba yalikuwa ndiyo sababu ya kuporomoka kwa uchumi
wa taifa hilo.Bei za vyakula na bidhaa mbalimbali zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya
juu, na inasemekana maisha ya wazimbabwe yamekuwa ni magumu.
Kiongozi wa chama cha upinzani, Morgan Tsavangirai aliyewahi
kushindana na Mugabe katika medani za siasa, hakuweza kufaulu kumuondoa
madarakani Rais Robert Mugabe.Kulikuwa na madai kwamba Morgan Tsavangirai
alikuwa ni kibaraka cha mataifa ya nchi za ulaya ya Magharibi. Katika mojawapo
ya hotuba zake kwa wale waliokuwa wakimtaka aondoke madarakani, Robert Mugabe
alikuwa akisema kwamba asingeweza kukubali kumwachia nchi yake ya Zimbabwe ‘
kibaraka’ ambaye hajui mateso ya wakombozi wa Zimbabwe walipokuwa wakipigana
vita msituni.Inawezekana kitu kinachompa mashaka kiongozi huyo ni mapenzi yake
ya dhati dhidi ya nchi yake. Anajiuliza, je, haitatokea kwa kiongozi
atakayechukua nafasi yake kuirejesha tena kwa wakoloni? Maswali hayo yanamnyima
raha
Inawezekana kabisa kwamba wazimbabwe walikuwa wamemvumilia
Robert Mugabe, lakini maamuzi yake ya kutaka kumrithisha mke wake Grace, ndiyo
yanayozidisha chuki ya wazimbabwe dhidi yake. Na hilo ni kosa kubwa na baya
kabisa kwa kiongozi kuifanya familia yake kuendelea kutawala kana kwamba
inatawaliwa kifalme.Wanaopinga utawala wa Robert Mugabe wanasema taifa hilo
sasa lilikuwa linaongozwa na mke wake Grace kiasi kwamba hata hotuba zake
alikuwa hawezi kuziandaa.
Ni katika hali ile ile kwamba viongozi na wanachama wa
ZANU-PF hawakubaliani Grace ampokonye cheo aliyekuwa makamu wa Rais,Emerson
‘Mamba’ Mnangagwa. Grace hakubaliki kwa kuwa hakutoka jasho la kuikomboa
Zimbabwe kutoka kwa wakoloni kama ilivyo kwa Mnangagwa.
Ingawaje walio wengi wanamtaka Robert Mugabe aondoke
madarakani, lakini atakumbukwa kwa msimamo wake usiolegalega hususan kwa
mataifa ya Ulaya.Aliweza kuthubutu kuyaambia bila woga yaache kuingilia masuala
ya waafrika. Mpaka sasa Rais Mugabe ni miongoni mwa viongozi wa serikali ya
Zimbabwe waliozuiliwa kuingia katika nchi za Ulaya.
Mwananchi mmoja akiwa nchini Zimbabwe na kuhojiwa na Shirika
la Utangazaji la Uingereza (BBC) akizungumzia kuhusu mgogoro wa kisiasa nchini
humo, alisema wao walikuwa wamemzoea(Robert Mugabe) kwa hali hiyo hawakuwa na
uhakika atakayefuatia utawala wake utakuwaje.Wengine waliohojiwa walisema
walikuwa wanapenda mgogoro huo umalizike kwa amani wakitaka kiongozi huyo apewe
heshima zake za kuikomboa Zimbabwe hadi kuwa huru hapo mnamo mwaka 1980.
Wapo waliouchukulia mgogoro wa utawala wa Zimbabwe kuwa
umekuwa fundisho kwa viongozi wengine barani Afrika wasipende kukaa madarakani
kwa muda mrefu. Waliwataja marais wa Uganda,Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo kwamba ni wakati muafaka kwao kujifunza kutokana na kile kilichotokea
nchini Zimbabwe, na wakubali kuondoka
madarakani mapema.
Nchini Uganda, Rais Yoweri Kaguta Museveni kipindi chake cha
kuwa Rais kimefikia ukomo, lakini amekuwa akishinikiza kupitia kwa wabunge ili
muda wake uongezwe. Naye Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amekuwa
akikwepa kufanyika kwa uchaguzi. Hali hiyo inaendelea kusababisha maandamano ya
wananchi wanaotaka uchaguzi huo ufanyike na apatikane kiongozi mwingine. Rais
Paul Kagame wa Rwanda, naye vile vile amekuwa akishawishi mabadiliko ya katiba
yanayomhalalisha yeye kuendelea kutawala.
Hakuna shaka kwamba Rais Robert Mugabe ataondoka madarakani
kwa kuwa wazimbwe wanamtaka afanye hivyo, lakini haitakuwa vyema kama
wazimbabwe hao watayasahau yale mema yote aliyoifanyia nchi yake.Inawezekana
pamoja na mageuzi ya uongozi ya kupata kiongozi mwingine, siyo kwamba maisha ya
Wazimbwe yatakuwa bora zaidi. Yawezekana yakawa mabaya zaidi kuliko hata wakati
wa utawala wa Rais Robert Mugabe. Kama alivyozungumza mwananchi mmoja huko huko
Zimbabwe, walikuwa wamemzoea Robert Mugabe hawajui ajaye, atakuwaje. Dunia yote
inasubiri, lakini historia ya Wazimbabwe haiwezi kumsahau Robert Mugabe.Afrika
itamkumbuka kwa kuwa kiongozi jasiri aliyekataa kuburuzwa na mataifa ya Ulaya
yanayowataka viongozi wa kiafrika kufanya watakavyo.