Saturday, January 20, 2018

CHADEMA MSIPATE KIGUGUMIZI KUKUBALI KUKUA KWA UCHUMI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kimempinga mwanachama mwenzake, Waziri Mkuu mstaafu Edward  Lowassa aliyeisifia serikali ya awamu ya tano kwa kuwaletea maendeleo wananchi wake. Edward Lowassa alikwenda Ikulu na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufulil

Kwa mfano, Lowassa alisifia ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza na Kigoma. Vile vile mradi wa bomba la mafuta kutoka nchini Uganda hadi mkoani Tanga. Lowassa aliitaja miradi hiyo kuwa itapanua wigo wa ajira hapa nchini na kuongeza kipato.

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe anasema alichokizungumza Lowassa huko Ikulu siyo kauli ya chama chao. Licha ya kutokuwa kauli ya chama chao, Mbowe alimshangaa Lowassa kwa kutolizungumzia suala la kushambuliwa kwa kupigwa risasi mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu. Baadaye mbunge huyo alipelekwa kwenye hospitali ya Nairobi nchini Kenya.Kwa sasa amehamishiwa nchini Ubelgiji kuendelea na matibabu.

Mbowe vile vile anasema watanzania wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha, iweje Lowassa asifie serikali kwamba hali ya uchumi ni nzuri ama inaridhisha? Naye Lissu anapinga akisema Lowassa hakupata kibali cha chama chao ili aweze kwenda Ikulu na kuzungumza na Magufuli.Mbunge wa Arusha, Godbless Lema hakubaki nyuma kumlaumu Lowassa kwenda Ikulu kumsifia Magufuli

Ni ukweli usiopingika kile kilichozungumzwa na Lowassa kwa Magufuli hakikuwafurahisha viongozi wa CHADEMA. Lakini Edward Lowassa ambaye amewahi kuwa kada wa chama cha Mapinduzi na kiongozi wa ngazi ya juu serikalini, alikuwa na haki ya kupangilia kipi cha kuzungumza anapokutana na kiongozi wa nchi.

Isingekuwa ni busara kwa Lowassa kuzungumzia suala la kushambuliwa kwa Lissu kwa Magufuli Lowassa anafahamu kuwa tayari serikali ilikuwa imelitolea ufafanuzi wa kuendelea na uchunguzi na upelelezi ili kuwanasa waliohusika. Hata kama angethubutu kulihoji angejulishwa alipeleke kwa mkuu wa jeshi la polisi kwani kwa wakati huo haikuwa mahali pake.

Kwa hali hiyo basi, kama angethubutu kulihoji ama kuliulizia lingemfedhehesa na lingeharibu ladha ama mantiki ya kwenda Ikulu.Hoja hiyo ingemsababishia Lowassa atambulike kama ni kiziwi ama jeuri kwani haikuwa nafasi ya kurudiarudia maneno yaleyale.

Ama kwa awamu hiyo ya kwanza hakuyazungumzia, yanaweza kuzungumzwa kwa awamu ijayo kwani uwezekano wa Lowassa kurudi  Ikulu bado atakuwa anakaribishwa tena.Lowassa kama  mwanasiasa ndiyo kwanza amefungua ukurasa mpya wa kukutana tena na kubadilishana mawazo na Magufuli.

Ni kweli Lowassa aliwachukiza viongozi wa CHADEMA eti kwa kusifia na kupongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuimarisha uchumi. Sasa viongozi wa CHADEMA walitegemea akanushe ama apuuze taarifa za wataalalmu wa uchumi kwamba uchumi unakua?  Walitaka awasilishe porojo kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli? Na kwa ujasiri na umakini wa Dk. Magufuli,angekubali? Isingewezekana

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu hivi karibuni Profesa Beno Ndulu.amewathibitishia watanzania kwamba uchumi wa nchi unakua. Gavana huyo kwenye taarifa yake alitoa vigezo mbalimbali vinavyothibitisha kukua kwa uchumi.Mojawapo ya vigezo hivyo ni vya huduma za fedha ambavyo vimekua na kuongezeka.
Hata kabla ya kutolewa kwa taarifa ya Gavana Ndulu, Rais Dk.Magufuli alikuwa akiwaeleza watanzania kwamba uchumi wa Tanzania unakua. Amekuwa akibezwa na wapinzani kumfanya kiongozi wa nchi aonekane mwongo.
Uthibitisho wa Gavana Ndulu, unaungwa mkono na msemaji wa serikali Dk. Abbas ambaye naye anaitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano za Afrik ambazo uchumi wake unakua na kusitawi. Hivyo basi malalamiko ya viongozi wa CHADEMA yaliyomtaka Lowassa azungumze tofauti na taarifa za wataalamu, yanawatambulisha waonekane kuwa viongozi wasiopenda kusema ukweli hata pale ambapo umethibitishwa.

Na kwa kuwa viongozi hao wa CHADEMA hawataki kuukubali ukweli huo, wanawekwa kwenye kundi la maadui wa usitawi wa uchumi wa Tanzania. Kauli hiyo ilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Magufuli alipokuwa akimuapisha Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko.

Magufuli anasema kwa wakati huu tuko mapambano makubwa na vita vya kiuchumi. Siyo kila mtu ama taifa litakuwa linafurahishwa na mapambano hayo. Lakini sasa tumeanza kuwasikia maadui wa vita hivyo hapa hapa nchini,hususani unapopatikana ushindi.

Kwamba siyo ajabu wakati watanzania tukijivunia ama kujipongeza kwa mafanikioa hayo, kundi jingine la watanzania wenzetu linaichafua ili watanzania wasipata nafasi ya kujipongeza kwamba wanafanya vizuri kiuchumi.

Kukua kwa uchumi hapa nchini kunaashiria mwitiko wa wananchi kufanya kazi kwa bidii ya kulijenga taifa lao. Lakini vile vile kukua kwa uchumi kunatokana na usimamizi wa kudhibiti ubadhirifu wa rasilimali za umma, rushwa na ufisadi. Imani ya wananchi kwa serikali yao kwamba inawatumikia na kujali maslahi ya umma, vinawapa faraja ya kushirikiana serikali yao.

Kwa upande mwingine ni ujasiri na moyo wa kizalendo unaooneshwa kwa vitendo na Rais Dk. Magufuli. Amekuwa mstari wa mbele kukataa kutafuta kujineemesha ama kujitajirisha yeye binafsi. Ameweza kutoa uthibitisho h uo katika kusimamia rasilimali za madini kwa kuzibana kampuni kulipa kodi.Ameweza kuonesha ujasiri huo akiwatetea watanzania ambao wamenyonywa kwa muda mrefu na kuwasababishia kuwa maskini.

Kwa kuwa wenzetu hawako pamoja nasi katika kujipongeza kwa usitawi wetu wa uchumi, hatutawashangaa tukiwasikia wakiwashawishi watu wafanye hujuma dhidi ya ustawi wa uchumi huo.Watafanya hivyo kwa kuwachanganya kwa taarifa zao kama wanavyofanya sasa. Inakuwaje uelewa wao unakuwa mdogo wanapopewa taarifa ambazo ziko wazi kwa manufaa ya watanzania?

Hivi hao wanaozikataa taarifa hizo za kukua kwa uchumi wa Tanzania, wanataka wao ndiyo wawe watoaji wa taarifa za hali ya uchumi wa taifa hili? Hilo kamwe haliwezekani.Wao ni vyema waendelee na siasa ambako wanaweza kufanya ubabaishaji, lakini siyo kwenye utaalamu kwenye hali ya  kiuchumi.

Ama kama wanata wajipe madaraka hayo, basi ni vyema wakawafanyia wanachama wao ambao wataendelea kubaki nyuma kwa kupewa taarifa ambazo hazioneshi mabadiliko. Watanzania wapenda maendeleo wanayo shauku ya mabadiliko.Hawazipendi taarifa za kushindwa. Ni wakati wao kutembea kifua mbele kujipongeza kwa kukua kwa uchumi wao.