Yatakuwa ni maumivu makubwa kwa wanachama wabadhirifu wa
Chama cha Mapinduzi kwa kulia na kusaga meno. Kamwe haitavumilika mali
za chama kufujwa, kuporwa ama kuhujumiwa na wajanja wachache. Hivyo ndivyo sasa
Mwenyekiti wa chama hicho Dk. John Pombe Magufuli alivyoanza katika mkakati
wake madhubuti wa kutaka mali
za Chama cha Mapinduzi zote zihakikiwe.
Uhakiki wa mali
zote za Chama cha Mapinduzi unalenga kutaka kujua ziko wapi na ni nani
anazimiliki, na je kinachopatikana kinafikishwa kwenye chama? Wale waliokuwepo
miaka ya sabini na themanini wanaikumbuka baadhi ya miradi iliyokuwa
imeshamiri. Kwa kutaja michache, pale Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam kulikuwa na duka kubwa la
bidhaa mbalimbali. Haikufahamika ni katika mazingira gani duka hilo halikuweza
kuendelea..Kuna majengo mengi yaliyopangishwa ambayo inadaiwa yanawanufaisha
wajanja wachache. Kwa ujumla Chama cha Mapinduzi kimekuwa na rasilimali nyingi
ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kuporwa na kusababisha kishindwe kujiendesha na
kutegemea kusaidiwa na serikali.
Kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi wanaokitumikia kwa haki
bila kutafuta kujitajirisha, wataupongeza msimamo huo wa Mwenyekiti wao ambao
ni wa kukijengea heshima kubwa. Kwamba
wanachama wachache ambao walikabidhiwa dhamana ya kusimamia mali za chama hawakujali kuzitunza.
Ni hali ambayo ilisababisha kujenga matabaka miongoni mwa wanachama.Isingekuwa
rahisi kwa chama kuwa na lugha moja katika kuwaongoza wanachama wake.
Ni dhahiri uhakiki huo wa mali
za chama, hautotofautiana sana
na uhakiki wa watumishi uliofanyika katika taasisi za serikali. Ulilenga
kujiridhisha kuhusiana na idadi yao pamoja na
uhakika wa elimu zao kama zilipatikana kupitia
mfumo rasmi unaotambulika serikalini.Matokeo ya uhakiki huo yaliweza kubaini
kasoro mbalimbali.
Waligundulika watumishi wengi ambao walighushi viwango vya
elimu.Ilibainika kulikuwa na watumishi waliokufa na watoro waliokuwa
wakiendelea kulipwa mishahara.Kasoro hizo zilikuwa zikiigharimu serikali kulipa
fedha nyingi na kuisababishia hasara kubwa.
Chama cha Mapinduzi ni tajiri. Hiyo ni kauli ya Mwenyekiti
wake Dk. John Pombe Magufuli aliyoitoa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama.
Anasema dhamira yake kubwa ni kuhakikisha kinajiendesha katika shughuli zake badala ya kutegemea misaada kutoka
serikalini ama wafadhili wengine.
Kuna hatari kubwa kwa chama kama
kitategemea misaada kutoka kwa wafadhili. Wanaweza wakawa watu binafsi ama
mataifa fulani. Kama ni mtu binafsi
amekisaidia chama, ni rahisi kukilazimisha chama kifanye kulingana na matakwa
yake. Hali kadhalika kama ni mataifa mengine,
yanaweza yakakilazimisha chama kitekeleze itikadi zake tofauti na zile za chama
chenyewe.
Tumekuwa tukisikia utegemezi wa chama kutoka kwa wafadhili wakithubutu
hata kumchagua mgombea wamtakaye. Hali hiyo imekuwa ni hatari kubwa kwa
kuwakosesha wanachama kuwa na nguvu katika chama chao.
Hata wale wanaomsikia Mwenyekiti Dk. John Pombe Magufuli
katika hotuba zake, anajisifu kwamba yeye hakufadhiliwa na mtu yeyote.Hakufanya
hivyo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Na ujasiri wake wa
kuiongoza serikali na Chama cha Mapinduzi, anabainisha unatokana na yeye
kujisimamia na kukubalika kwa wanachama wake bila ya kutumia ushawishi
mwingine.
Wale wote waliofuja ama kuficha mali za chama kwa kujisahau, wakati
umefika kuzisalimisha ama wao kuwajibika.Wapo watakaolazimika kuadhibiwa
wakithibitika kuhusika na makosa hayo.Yote hayo yanafanyika kwa lengo la
kukisafisha chama hicho.
Ni mageuzi ya kishindo yanayofuatiliwa na wengi kutoka ndani
na nje ya nchi. Ndiyo hayo yanayowakurupusha kutoka upinzani na hatimaye kujiunga na Chama cha Mapinduzi. Haiwezekani
utitiri wa wanachama ukarejea Chama cha Mapinduzi, kama
hakuna kazi nzuri inayofanyika.
Ni vyema kabisa kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi
wakayaunga mkono kwani yana tija kwa chama chao.Japokuwa baadhi watakuwa
wanaumia, hivyo ndivyo ilivyo katika harakati zozote za kuleta mageuzi ya
chama.
Maelekezo ya Dk. John Pombe Magufuli kwa kamati aliyoiunda
katika uhakiki wa mali za
chama, utawahusu hata wanachama walioko serikalini ambao watahojiwa kuhusiana
na mali
za Chama cha Mapinduzi.
Matokeo ya awali ya mageuzi hayo ni ongezeko la wanachama. Lakini
vile vile yapo matumaini makubwa yatakayofuatia ambayo kila mwanachama
atayafurahia. Chama kitakuwa na uwezo mkubwa wa kujiendesha bila ya kutegemea
ama kuombaomba misaada kutoka mahali popote.
Kuna uhusiano wa waziwazi wa dhamira ya Dk. John Pombe Magufuli kusafisha uozo wote
serikalini na ndani ya Chama cha Mapinduzi .Hali kadhalika siyo rahisi kukiacha
chama cha Mapinduzi kikibaki na genge la wezi,wafujaji na mafisadi. Serikali
iliyoko madarakani inatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Ingekuwa siyo haki na wala kutoa taswira sahihi kama
usafishaji wa uozo huo ukabakia serikalini peke yake. Chama cha Mapinduzi kwa
nafasi yake ya kuwa madarakani kwa muda mrefu, kinastahili kuonesha mfano wa
kuzingatia maadili ya kutotiliwa mashaka.
Siyo muda mrefu wanachama wa Chama cha Mapinduzi watakwenda
kwa wanachama ifikapo mwaka 2020, kwenda kuomba kura na kuwanadi wagombea wao. Sifa pekee itakayowavutia
wapiga kura ni kuyatangaza mageuzi hayo yatakayokuwa yamefanyika na
kuwanufaisha.
Kwa mfano kuna matukio ya dhati kabisa ambayo wanachama wa
Chama cha Mapinduzi wameyashuhudia. Katika uchaguzi wa viongozi wa Umoja wa
vijana wa Chama cha Mapinduzi, ilidhihirika jinsi rushwa ilivyodhibitiwa
kikamilifu. Mwenyekiti aliyekuwa anamaliza muda wake wa uongozi aliweza
kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa.
Kwenye jimbo la uchaguzi la Singida Kaskazini, mgombea mmoja
wa kiti cha ubunge alikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa(TAKUKURU) kwa tuhuma za kutoa rushwa kwenye kura za maoni. Alifikishwa
mahakamani na yuko nje kwa dhamana. Hizo ni jitihada za makusudi kabisa za
kuhakikisha wagombea wote ndani ya Chama cha Mapinduzi hawapatikani kwa kutumia
fedha ama ghiliba za aina nyinginezo.
Imani ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi kwamba hata asiye
na fedha, imeanza kurudi kama ilivyokuwa
wakati wa utawala wa hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nyerere aliwachukia wanachama waliokuwa
wakitumia fedha ili kununua uongozi. Hakusita kuwafukuza wanachama wote
waliokuwa wakitumia fedha ili kuingia madarakani.Kwa wakati wake chama
kiliheshimika na kutumainiwa. Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wanaamini sasa
Dk. John Pombe Magufuli atakirudisha Chama cha Mapinduzi kwenye heshima yake.Kitaendelea
kuheshimika ndani na nje ya Tanzania .
