‘samahani’ ama kuomba msamaha’(kusamehewa) ni
kukiri,kukubali ama kuomba radhi kwamba kuna tendo lisilofaa lililofanyika na
kumfanya binadamu mwingine ajisikie vibaya (kuchukizwa)kuumia, kusumbuka ama
kukerwa.
Kwa mfano wa kawaida, imekuwa ikisikika kwa Shirika la Ugavi
wa Umeme (TANESCO)kuwaomba radhi ama msamaha pale huduma zake zinaposababisha
usumbufu,ama uharibifu kwa wateja wake. Ama hata Shirika la Reli (TRL)
inapotokea kuwa kuna matatizo yanayosababisha ratiba ya usafiri
kubadilika,taarifa ya mabadiliko hayo hutolewa na kisha kufuatiwa na kuwaomba
radhi (msamaha) wateja wao. Maneno hayo yanapojumuishwa na neno ‘samahani’
mahali popote hutoa ishara ya kutambua na kutaka kujenga uhusiano mwema kati ya
pande mbili zinazoshirikiana katika kufikia malengo yao.
Mathalani, mtu anaweza kutamka maneno ambayo binadamu
mwenzake yanaweza kumsababishia kupoteza heshima yake na kudharauliwa.
Ukimtakia mwenzako kwamba akili zake ni sawa na Mbwa,itamchukiza na kumkera.
Kwa kutambua kuwa amechukizwa ama kukerwa na maneno hayo,mtu muungwana
atachukua hatua ya kuomba msamaha kwa yule aliyemtamkia maneno mabaya.Wapo
binadamu ambao wakiombwa msamaha wanakubali kwa kutamka maneno kwamba
wamemsamehe aliyewafanyia yale yasiyofaa. Lakini wapo wengine wanaodiriki
kutamka kwamba ‘wanasamehe’ lakini hawatasahau.
Wapo baadhi ya watu ambao wanaweza kuwaomba msamaha ama
radhi wale waliowakosea wakiwa wanaonana ana kwa ana. Wapo wengine ambao hukosa
ujasiri na huwatumia ndugu zao kuomba radhi ama msamaha.
Katika vitabu vitakatifu kama vile Biblia, umuhimu wa
kusamehe ama kuomba radhi vinasisitizwa katika imani ya wakristu.Katika kitabu
hicho kitakatifu, Yesu Kristu alipokuwa akifanya kazi ya kuhubiri aliulizwa ni
kwa kiwango gani mkristo anatakiwa amsamehe mwenzake? Yesu Kristo aliwajibu
kuwa ni saba mara sabini.Wakristo katika mafundisho ya imani yao wanahimizwa
kuwasamehe wale wote wanaowakosea bila ya kikomo.
Kupenda kusamehe ni dawa ya afya mwilini. Kushindwa kusamehe
ni kuhifadhi sumu mwilini. Padre John Kulwa kutoka Seminari Kuu ya Kanisa
Katoliki Segerea katika jimbo la Dar es
Salaam alisisitiza umuhimu wa kusameheana wakati wa mahubiri yake kwa waumini
wa Kigango cha Buyuni jijini Dar es Salaam. Alisema kulikuwa na matukio mengi
ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipata matatizo makubwa ya kiafya, kisha
kupelekwa Hospitali na kuuguzwa ambapo baadaye hugundulika kuwa chanzo chake ni
kukataa kuwasamehe wenzao. Kwamba wanapoamua kuwasamehe wenzao,matatizo yao
yanakoma.
Hapa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM)chini ya
Mwenyekiti wake Dk. John Pombe Magufuli tuliona kikitoa msamaha wa kumrejeshea
uanachama Sophia Simba aliyekuwa amefukuzwa.
Sophia Simba aliwahi kuwa waziri kwenye serikali ya awamu ya
nne na pia kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT). Aliwahi kuwa
mjumbe wa vikao mbalimbali vya Chama Cha Mapinduzi, kama vile Halmashauri
kuu.Naye kama katika makala hii inavyojadili, alitambua kuwa alifanya jambo
ambalo halikuendana ama lilikiuka maadili ya chama chake hadi kufikia kufukuzwa
uanachama.
Katika kutambua kosa lake, Sophia Simba anakiri na kuomba
radhi(msamaha) kwa Mwenyekiti wa Chama chake kwa kumuandikia barua. Yeye
mwenyewe anaelezea athari alizozipata kutokana na makosa yake. Anakiri zaidi
kuwa maisha yake na mafanikio aliyoyapata yametokana na yeye kuwa mwanachama wa
Chama cha Mapinduzi. Nao wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi
kilichoketi Ikulu jijini Dar es Salaam walikubali kwa kauli moja kumsamehe
Sophia Simba kwa yale yaliyotokea. Sophia Simba anakiri kuwa atakuwa mwanachama
mwaminifu na mtiifu kwa viongozi wake. Ni dhahiri msamaha wa aina hiyo unatoa
fursa ya kuanza ukurasa mpya wa kukijenga chama kipya.Katika maandalizi ya
uchaguzi utakaofanyika hapo mnamo mwaka 2020, nguvu yake inahitajika zaidi
katika kukipa ushindi wa kishindo Chama cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya vyama vya
upinzani.
Msamaha huo kwa wanachama wake unajenga imani kwa wanachama
wake kuwa pale wanapokosea wanaweza kusikilizwa na kisha kusamehewa. Msamaha ni
afya katika kujenga na kuimarisha uhusiano wa watu lakini vile vile hata katika
taasisi kuna umuhimu wa msamaha.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa madaraka
kwa Rais aliye madarakani, kutoa msamaha kwa wafungwa walioko gerezani. Ni
wakati wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika Rais Dk. John
Pombe Magufuli alitoa msamaha. Wafungwa zaidi ya 8000,walisamehewa vifungo vya
maisha, kunyongwa ama kupunguziwa muda wa kukaa gerezani.
Hata nje ya Tanzania yapo mataifa kadhaa ambayo yamewahi
kusikika yakiomba msamaha kutokana na makosa yaliyofanywa na kusababisha
madhara kwa watu wengine. Matamshi hayo yamekuwa yakichukuliwa kama ishara ya
kujutia yaliyotokea na kutaka kujenga uhusiano mwema na imara.