Mwanamuziki maarufu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,
Koffi Olomide hivi karibuni ametunga wimbo wa kuwaomba radhi wanawake wote duniani. Umepewa jina la ‘pardon’.
Mwanamuziki huyo anasikika akitaja maneno kwa lugha ya Kiswahili, ‘ninaomba
radhi’. Kwa mujibu wa matangazo ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC)
Koffi Olomide anawaomba radhi wanawake kufuatia kitendo cha udhalilishaji
alichomfanyia mwanamke mmoja wa wachezaji(wanenguaji) wake alipofanya ziara
yake ya kutumbuiza nchini Kenya miaka michache iliyopita. Katika tukio hilo,
mwanamuziki Koffi Olomide alimpiga hadharani kwa kumuonea. Alilaaniwa na wengi.
Serikali ya Kenya kwa kuchukizwa na udhalilishaji huo, ilimfukuza na kufuta onesho la muziki
lililokuwa limepangwa kufanyika nchini humo.
Nayo serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilimpa
adhabu ya kifungo, hata hivyo Olomide hakuweza kuitumikia adhabu hiyo katika
hali ya kutatanisha. Kuzembea kwa utekelezaji wa adhabu hiyo kulitoa picha ya
upendeleo dhidi ya mwanamuziki huyo. Hakuna uhakika kama wananchi wengine wa
kawaida nchini humo wangeweza kupata upendeleo kama alivyofanyiwa Koffi
Olomide. Baadhi ya wanawake waliohojiwa na Shirika la Utangazaji la
Uingereza(BBC) walisema Koffi Olomide hastahili kusamehewa kwani udhalilishaji
aliomfanyia mwanamke mwenzao haukubaliki. Walisema mwanamke ni kiumbe cha
thamani kubwa kinachostahili kuheshimiwa na kutunzwa na wala siyo kuonewa na
kudhalilishwa.
Lakini wanaume nao waliohojiwa nchini humo kuhusiana na
wimbo wa msamaha huo, wanasema Koffi Olomide anastahili kusamehewa kwa kuwa
ameomba radhi na amekiri na kujutia kosa lake. Ingawaje Koffi Olomide amewaomba
radhi wanawake,serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ilifanya kosa kwa kushindwa
kumuadhibu wakati serikali za mataifa mengine zilikuwa zimetoa adhabu ama zilionesha kukera na udhalilishaji huo.
Serikali ya Zambia nayo ilifuta maonesho ya mwanamuziki huyo, ikionesha
kuchukizwa na kukerwa na udhalilishaji huo.
Wanawake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanapoukana
msamaha wa Koffi Olomide, wanatafakari kwa kile kilichofanywa na serikali yao.
Bado wanayo hofu kubwa kwamba inawezekana Koffi Olomide akarufia kosa kama
hilo, siyo ajabu serikali yao ikashindwa kuungana nao katika kutetea heshima na
utu wao.
Koffi Olomide ametekeleza wajibu wake wa kuonesha kujutia
kitendo kibaya na kiovu alichomfanyia binadamu mwenzake. Ingawaje siyo wanawake
wote wanaoukubali msamaha wake, anachotakiwa kufanya ni kuwathibitishia
wanawake wote kwamba hatarudia tena kuwanyanyasa wanawake. Wanawake popote
walipo ni sawa na Mama yake,dada,shangazi,bibi na mke wake. Hakuna uhalali
wowote wa kutumia nguvu kuwanyanyasa. Wanastahili mapenzi na kuthaminiwa utu na
heshima zao. Kama wanawake hao wanamuudhi kwenye muziki wake,atumie busara na
hekima.