Tuesday, January 02, 2018

Kamati maalum itachunguza mikataba ya uagizaji wa magari yaliyoko bandarini



By Bakari Kiango, Mwananchi; bkiango@mwananchi.co.tz
Dar  es  Salaam. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi  Hamad Yusuf  Masauni amesema ataunda  kamati ya wataalamu kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa magari yote ya polisi 119 yaliyopo bandarini na  53 ya Chuo cha Mafunzo cha Polisi Kurasini.
Mhandisi  Masauni amefikia uamuzi huo  baada ya kubaini magari matano kati ya 53 ya Chuo cha Mafunzo cha Polisi Kurasini yana hitilafu mbalimbali.
Naibu Waziri huyo, ameeleza hayo leo Jumanne,  Januari 2, 2018 wakati alipofanya ziara ya kukagua magari hayo katika maeneo ya bandarini na katika chuo hicho.
Amesema kamati hiyo itajumuisha wataalamu mbalimbali kutoka na idara mbalimbali za Serikali ili kuja na majibu ya kina kuhusu hitilafu hizo.
Mhandisi Masauni amesema bandarini kuna magari ambayo ni malori, hivyo kamati  hiyo itachunguza mikataba ya uagizaji wa magari hayo kwa kuwa ni aina moja wakati polisi inauhitaji wa aina mbalimbali za usafiri.