Tuesday, January 02, 2018

WANAOWAKATISHA MASOMO WATOTO WA KIKE KWA MIMBA HAWASTAHILI HURUMA

Image result for Profesa Joyce NdalichakoSerikali imekuwa ikichukua hatua kali na madhubuti za kulinda maendeleo ya watoto wa kike hususan wanapokuwa shuleni, lakini inakatishwa tamaa na tabia mbovu za baadhi ya wazazi.dadi ya watoto wa  kike wanaokatisha masomo yao kwa matatizo ya kupata ujauzito, inatisha.Wazazi wamekuwa wakishiriki kuwaficha wanaume wanaowapa ujauzito watoto wao wa kike,kwa kuelewana na wahalifu badala ya kuwashitaki mahakamani na kuadhibiwa.Nchini Tanzania ni kosa kisheria kwa mwanaume kumpa ujauzito mwanafunzi wa kike. Adhabu yake ni kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Ingawaje kwa muda mrefu elimu ya kuwalinda watoto wa kike imekuwa ikitolewa,ni kama vile wazazi wanaziba masikio. Wamekuwa wakiendelea kuwafanya watoto wa kike kuwa kitega uchumi. Imekuwa inashangaza khata wakati wa kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya shule ya msingi,wazazi wamekuwa hawapendi watoto wao wa kike waendelee na masomo.

Kwa mfano huko mkoani Tanga kulikuwa na taarifa ya kushangaza. Walichokifanya wazazi ilikuwa ni kuwalazimisha watoto wao wa kike wajibu vibaya maswali ya mtihani.Walikuwa wakifanya hivyo ili kuwazuia watoto wa kike wasiendelee na masomo kisha kukosa mahari.

Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Joseph Kakunda awakilisha hisia za serikali na wote wapenda maendeleo ya watoto wa kike kwamba tatizo hilo halivumiliki.

Takwimu za watoto wa kike wanaopata ujauzito na kisha kukatisha masomo zinasikitisha. Aidha hata utaratibu wa kuwaadhibu wanaume wanaofanya makosa hayo zinawapa fursa ya kukwepa adhabu. Mathalani, mtuhumiwa anapopewa haki ya kupewa dhamana anapofikishwa mahakamani wakati mwenendo wa kesi ukiendelea umekuwa ukichangia kuendeleza uhalifu dhidi ya watoto wa kike.

Endapo mapendekezo ya Joseph Kakunda ya kuwasilisha bungeni ili kuondoa dhamana kwa wakosaji hao yatapitishwa,yanaweza kupunguza ama kukomesha kabisa na kulinda ustawi wa watoto wa kike. Serikali inawaonea huruma watoto wa kike wanaokatishwa masomo yao, lakini inashangaza wazazi hawajali wapowaficha wahalifu.

Msomo mmoja aliwahi kuandika kwamba unapomuelimisha mtoto wa kike, ni sawa na kulielimisha taifa zima. Hakuna sababu yoyote iwayo inayoweza kuikataza serikali isiwatetee watoto wa kike wanaokoseshwa masomo yao. Serikali inawategemea sana watoto wa kike katika kuleta mabadiliko ya kuleta maendeleo hapa nchini.

Wakati fulani katika kujadili namna ya kukabiliana na tatizo, hilo imekuwa ikipendekezwa adhabu kali itolewe kwa wazazi wanaowaficha wahalifu. Kwa mfano,mzazi mmoja wa mtoto wa kike anamficha mhalifu ilhali anamfahamu, anapaswa na yeye afikishwe mahakamani kwa kosa hilo na kisha kuadhibiwa.

Tatizo la kukatisha masomo watoto wa kike, halielekei kupata tiba. Lakini kwa upande mwingine kumekuwa na huruma ya kuwaadhibu wahalifu hao kwa kuwa  ni ndugu wa karibu, au kutokujali ustawi wa maisha ya watoto wa kikel. Hakuna sababu ya msingi ya kuwaonea huruma, bali waiache sheria ichukue mkondo wake na watoto wa kike waendelee na masomo. Tunatarajia kwamba hata mahakimu nao wawe shupavu katika kuzisimamia na kutoa adhabu hizo haraka pasipo kusubiri upelelezi wa muda mrefu/