Inawezekana ikawa ni fahari kubwa kwa kiongozi wa dini,
Zacharia Kakobe kutamka kuwa ana fedha nyingi kuishinda serikali ya Tanzania .
Kakobe anaweza kujidai ama kuwa na
ufahari huo kwa kuziona fedha hizo zikiwa zimerundikana kwenye mifuko ya rambo
ama zimetulia Benki. Ni nyingi kwa kadri ya uelewa wake. Hazina faida
yoyote kwa watanzania bali zimewekwa kama mapambo.
Matamshi ya Kakobe kuhusiana na kuwa na fedha nyingi, yana faida gani kwa watanzania
na serikali iliyoko madarakani?. Je,ni kejeli, ni demokrasia ama ni ukosefu wa
subira na hekima? Kuwa na fedha nyingi huku wengine hawanazo, kunaleta faraja
gani katika jamii?
Fedha za serikali siyo nyingi na wala hakuna ulazima wa
kuzitaja kuwa ni nyingi. Fedha za serikali hazipimwi kwa wingi. Fedha za
serikali zinapimwa kwa uwezo wake wa kuhudumia wananchi wake. Fedha za serikali
kamwe haziwezi kuwekwa zikatulia zikifanywa kama
mapambo, bali hugawanywa ili zitanzue matatizo ya wananchi wake.
Mojawapo ya sifa ya fedha za serikali ni kuona wananchi
wanavyonufaika nazo. Katika awamu ya tano ya serikali iliyoko madarakani,
imedhamiria kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Thamani ya
fedha za serikali ndivyo hivyo zinavyoweza kupimwa. Dalili za kufanikiwa kwa
mpango huo tayari zimeonekana. Idadi ya wanafunzi wanaojiandikisha kujiunga na
shule ya msingi, imeongezeka maradufu. Wazazi wanafurahia maamuzi hayo kwani
yamewaondolea kero za michango iliyokuwa ikiwanufaisha wajanja wachache.
Thamani nyingine ya fedha za serikali ni ulinzi wa wananchi
pamoja na mali
zao.Imeshuhudiwa wakati wa sherehe za Krismas na mwaka mpya wa 2018, Jeshi la
Polisi lilivyosimamia kuhakikisha kunakuwepo amani na utulivu. Jeshi la Polisi,
liliahidi kuimarisha ulinzi kwenye nyumba zote za ibada wakati wa sherehe hizo.
Hata mchungaji Kakobe asingeweza kutoa mahubiri yake kwenye kanisa lake, kama hali ya amani na utulivu ingekuwa siyo ya
kuridhisha.
Thamani nyingine ya matokeo ya fedha za serikali, ni pongezi
kutoka kwa wananchi wanaponufaika na huduma zitolewazo na serikali. Mathalani,
baada ya kumalizika kwa sherehe za Krismas na mwaka mpya 2018, wananchi
waliipongeza serikali kwa kuimarisha ulinzi. Wananchi hao walikiri kwamba
hapakuwa na matukio ya uhalifu kwenye maeneo yao na kwamba walisherehekea kwa amani.
Siyo jambo jepesi wala rahisi wanapojitokeza wananchi
kulipongeza jeshi la polisi kwa kusimamia amani, hususan katika mikoa yote
isiyopungua 26 ya Tanzania
bara. Serikali inafanya hivyo kwa kuwa inawathamini wananchi wake na
isingependa kuona ama kusikia uhuru na haki zao vinahatarishwa na watu wenye
nia mbaya.
Ilishuhudiwa katika kipindi hicho, ukaguzi wa magari ya
abiria ukifanyika kuhakikisha abiria wanasafirishwa na magari yaliyo imara.
Hizo zote ni gharama kwa serikali kwa kutumia rasilimali zake za muda na
wataalamu katika kulinda maisha ya wananchi wake.
Wakati wa majanga mbalimbali, tunaiona serikali ikijitokeza
kwa kuonesha thamani ya fedha zake kwao. Mathalani katika ajali iliyotokea
mkoani Arusha mwaka jana na kusababisha vifo vya wanafunzi, serikali iliweza
kugharimia mazishi na kutoa mkono wa pole kwa familia za wafiwa.
Mkoani Kigoma serikali iliweza kufanya hivyo hivyo.
Wanafunzi waliokuwa darasani na mwalimu wao, walipigwa na radi na kufariki hapo
hapo. Yamekuwa yakitokea matukio ya majanga ya mafuriko ya maji.Baadhi ya watu
wamekuwa wakifariki ama kupoteza makazi yao
ya awali. Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuokoa maisha yao .
Katika historia ya kuokoa maisha ya raia wake wa mkoa wa Dar
es Salaam , serikali iliamua kuwagawia wananchi eneo la
Mabwepande. Wananchi hao ni wale ambao walikuwa wanaishi eneo la
Jangwani,ambako ni bondeni na watu wengi wamekuwa wakisombwa na maji. Hata
hivyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakikaidi maelekezo ya serikali yanayolenga
kuokoa maisha yao .
Hapa jijini Dar es
Salaam kuna mradi wa mabasi yaendayo kwa mwendo wa
kasi. Mataifa mbalimbali yamekuwa yakifanya ziara za kikazi kuja nchini
kujifunza serikali inavyouendesha. Mradi huo wa mabasi unalenga kupunguza
msongamano wa magari na kuwawezesha wananchi kufika haraka kwenye shughuli zao
za ujenzi wa taifa. Hizo ni jitihada za dhati kabisa zinazothibitisha thamani
ya fedha za serikali kwa wananchi wake.
Tunazisikia jitihada za serikali katika kuwekeza kwenye
sekta ya afya. Serikali imedhamiria kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda
kutibiwa nje ya nchi.Wagonjwa watakaokwenda kutibiwa nje ya nchi ni wale tu,
watakaothibitika wameshindwa kutibiwa na madaktari wa hapa nchini. Taasisi ya
kutibu magonjwa ya moyo ya Jakaya Kikwete ni mojawapo ya viashiria vya
mafanikio katika sekta ya afya.
Madaktari bingwa wa taasisi hiyo kwa kushirikiana na
madaktari kutoka mataifa mengine wamethibitisha weledi wao mkubwa kwa kuweza
kutibu magonjwa ya moyo, figo na mengineyo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa
yakipoteza maisha ya watu kwa kiasi kikubwa. Taasisi ya magonjwa ya moyo ya
Jakaya Kikwete imeleta ukombozi wa kutibu magonjwa hayo katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.
Sambamba na hilo , serikali
hivi karibuni ilikifungua chuo cha mafunzo ya tiba, eneo la Mloganzila mkoani Dar es Salaam ili kuongeza idadi ya madaktari hapa nchini.
Yote hayo ni dhamira ya serikali katika kujali afya na uhai wao.
Serikali haioni fahari kuziona fedha zake hazifanyi kazi ya
kuwahudumia wananchi wake.Kila kukicha inaingia mikataba na mataifa mbalimbali
ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora.Kuna mradi mkubwa wa umeme
utakaojengwa huko Rufiji unaolenga kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme.
Kama hilo
halitoshi, Reli mpya ya kisasa inakarabatiwa kuanzia Dar es Salaam kuelekea
mikoa ya Kigoma na Mwanza. Abiria
watakaokuwa wakisafiri kuelekea mikoa hiyo watakuwa wakitumia wastani wa muda
wa saa nane hadi kufika kwao.Licha ya kwamba kutakuwa na unafuu kwa abiria,
lakini uharibifu wa barabara
unaosababishwa na magari yanayosafirisha mizigo mizito,utapungua.
Ikiwa mchungaji Zakaria Kakobe atakuwa naye ameyafanya kama
hayo yaliyofanywa na serikali, atakuwa amedhihirisha kwamba kweli anazo fedha
nyingi zaidi ya serikali.Hakuna mahali ambapo niliwahi kumsikia Kakobe akitajwa
ama kupongezwa kwa kuzitumia fedha zake kwa ustawi wa wananchi wa Tanzania .
Mathalani, yamekuwa yakijitokeza majanga ya kitaifa kama
vile mafuriko ama tetemeko. Sikuwahi kusikia akitoa mchango wake ili kuwanusuru
waathirika wa majanga hayo.Sasa madai yake kwamba ana fedha nyingi,
yanalisaidia nini taifa letu?
Kuwa na fedha na kisha kuziweka kwenye mifuko ya rambo ili
zionekane kuwa nyingi, pasipo kuwaletea ukombozi watanzania hakuna manufaa
yoyote bali hayo ni majigambo tu.
Kuna taasisi nyingi za kidini ambazo zimekuwa zikishirikiana
na serikali kuwahudumia wananchi. Taasisi hizo zimekuwa zikiwekeza kwenye huduma
za Afya, Elimu na nyinginezo.
Kitu ambacho mchungaji Kakobe alitakiwa kuwaeleza wananchi
ni vipi yeye amewekeza katika sekta mbalimbali ili kutoa huduma kwa wananchi. Kujigamba
kuwa yeye ana fedha nyingi zaidi ya serikali hakutakuwa na maana yoyote,
kinachotakiwa ni kuwaonesha wananchi kile alichowafanyia kulingana na fedha
zake. Na kama amefanya hivyo, kutakuwa na haja ya kulinganisha fedha zake kama zitakuwa
zinalingana na miradi mingi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali tangu kupatikana kwa uhuru mnamo
mwaka 1961.
Katika majigambo ya Kakobe, serikali yenyewe inaonesha kile
inachowafanyia kulingana na bajeti yake.Hata wananchi wenyewe wanakiona na
wananufaika.
