Monday, November 20, 2017

LAWRENCE MASHA AKIRI CHADEMA INAMJENGA MAGUFULI

Related image
Related imageMiaka miwili aliyokuwa amejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akitokea Chama cha Mapinduzi, Lawrence Masha amebaini CHADEMA kimeshindwa. Masha anasema wanachokifanya CHADEMA ni kumkosoa Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli hoja ambazo zinampa nguvu na kukubalika.Kwa maelezo ya Lawerence Masha,hakuna agenda nyingine yenye nguvu ya kisiasa ambayo inaweza kukihalalisha CHADEMA kuweza kutawala nchi kutoka mikononi mwa Chama cha Mapinduzi.

Lawrence Masha tayari ametangaza kukihama chama hicho.Kama ilivyokuwa kwa wanachama wengine wanaokihama Chama cha Mapinduzi na kujiunga na vyama vya upinzani,ndoto yake haikukamilika. Zilipotangazwa nafasi za wabunge wa Afrika ya Mashariki, Lawrence Masha alijitokeza kugombea kupitia CHADEMA. Hakuweza kuchaguliwa na wabunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inadhaniwa hiyo ingekuwa ni fursa ambayo angeitumia kukamilisha ndoto yake ya kuwa kiongozi. Sasa baada ya kuikosa nafasi hiyo, angeendelea kubaki CHADEMA ili iweje na yeye anaona uwezekano wa kutawala haupo?

Dosari pekee aliyojiwekea Lawrence Masha katika kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine, kunamfanya atiliwe mashaka hata kama atajiunga na chama kingine. Chama kitakachompokea kitakuwa na mashaka kuhusiana endapo atakuwa mwanachama wa kudumu. Anaweza kulinganishwa na tabia za popo.

Ni kumbukumbu nzuri na iliyotukuka kwamba angalau alipokuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi, alishika nafasi mbalimbali. Kwanza aliwahi kuwa mbunge. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya nne. Huyo ni mwanachama mwingine ambaye anawafuatia wanachama wengine waliourudi Chama cha Mapinduzi.Waliorejea miongoni mwao alikuwa ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida,Mgani Msindai na wenzake waliobaini udhaifu wa CHADEMA katika medani ya siasa. Na wao hawakuchukua muda mrefu kurudi kwenye chama chao cha awali.

Wanachama hao wanaojiondoa kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanasaidia kutoa somo kwa vyama vya upinzani,kwamba viachane na tabia ya kuikosoa serikali ya awamu ya tano vikidhani imeshindwa. Vyama hivyo vitambue waziwazi kwamba wananchi wanaziona juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kushughulikia matatizo waliyonayo ya muda mrefu.

Hebu fikiria jinsi wananchi waliokuwa  wamedhulumiwa haki zao za kuporwa viwanja na matajiri wanavyorejeshewa  kwa nguvu ya serikali.Tayari serikali ya awamu ya tano imetangaza kubomoa majumba yaliyojengwa kwa kuwadhulumu wananchi wanyonge.Tumemsikia mjane mmoja huko Mkoani Dodoma eneo la Msalato ambaye ardhi yake ilikuwa imeuzwa kwa ujanja kati ya mawakili na tajiri mmoja ambapo sasa mjane huyo amerudishiwa ardhi yake.

Lakini vile vile tunaziona jitihada za Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli katika kushughulikia matatizo ya wananchi anapofanya ziara zake za kikazi mikoani.Huko wananchi kutokana na imani kubwa waliyonayo kwake, wanamwelezea kile kinachowatatiza na yeye bila ya kupoteza wakati, anatoa suluhisho na majibu mara moja.Ni mwananchi gani katika hali kama hiyo ya serikali inavyowajibika kwa wananchi,ataichukia? Ama kwa vyama vya upinzani vitawaeleza nini wananchi ili washawishike kuvipa kura?

Kilichopo kwa sasa ni kwamba vyama vya upinzani vinapokea ruzuku ya bure ya uendeshaji ilhali hakuna jambo jipya linalofanywa kwa manufaa kwa wananchi.Haviwezi kusingizia kwamba vimekatazwa kufanya mikutano yake. Hiyo siyo sahihi hata kidogo kwani kama ni kufanya siasa, tangu mwaka 1992 vilikuwa vikifanya siasa.

Kama alivyobainisha Lawrence Masha kwamba medani za kukosoa serikali iliyoko madarakani, inazidi kuipa nguvu serikali ya sasa iliyoko madarakani. Kwa ukweli huo basi ni vyema vyama hivyo vikaamua tu kukubali na kutangaza kwamba kazi yao imekwisha. Vyama hivyo vinaelekea kupoteza mvuto kutoka kwa wananchi kwa kuwa hakuna mahali penye udhaifu wa serikali ya sasa. Kama kutakuwa na kasoro hiyo, basi itakuwa ni ile wanayoiona wanasiasa kutokana na upofu wao wa kuona na wala siyo wa wananchi wa kawaida.

Lakini kama inavyoeleweka kwa viongozi wa vyama vya upinzani,siyo rahisi kuamini viashiria hivyo vya wao kushindwa. Itakuwa ni vizuri wao kusubiri mpaka wakati wa uchaguzi ambako matokeo watakayoyapata yatawatia aibu.Ama  kwa upande mwingine, vyenyewe vikubali kuwa vyama vya kukisindikiza Chama cha Mapinduzi katika wakati wote kitakapokuwa kikishinda.

Sifa kubwa na ya kutosha inayokipa nguvu Chama cha Mapinduzi(CCM) mbele ya watanzania, ni kuwa na kiongozi ambaye ni mchapa  kazi. Sifa nyingine ni ya kuchukia vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma,ufisadi na rushwa. Katika kuwathibitishia watanzania kuwa anayo nia thabiti ya kuvikomesha watuhumiwa mbalimbali wameanza kushughulikiwa na mamlaka zinazohusika.Wapo waliofikishwa mahakamani na kuhukumiwa. Wapo waliohojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) wakitakiwa kutoa maelezo kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Lakini vile vile ni katika kipindi cha utawala huu wa serikali ya awamu ya tano ambapo wananchi wameshuhudia watuhumiwa wote wanashughulikiwa bila ya kuogopwa kutokana na nafasi zao katika jamii. Kwa mfano wananchi wamemshuhudia mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji akihojiwa Polisi kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya,kesi ya ubadhirifu wa fedha, kufikishwa Mahakamani na baadaye kuachiwa. Wananchi wa kawaida walikiona kitendo hicho kuwa cha kijasiri kwa serikali ya awamu ya tano kwamba haina mzaha. Kesi nyingine ambayo inaonesha serikali ya awamu ya tano haina mzaha, ni ile ya kampuni binafsi ya kuzalisha umeme (IPTL)ambayo kwa sasa inaendelea kusikilizwa mahakamani.Imekuwa ni ya muda mrefu, na iliaminika kwamba hakuna mtu wala serikali ambaye angeweza kuwashughulikia watendaji wa kampuni hiyo kujibu tuhuma za ubadhirifu dhidi yao kwa sababu ya utajiri wao. Watanzania wanawashuhudia watuhumiwa hao wakitakiwa watoe maelezo mahakamani.

Ujasiri kama huo wa serikali ya awamu ya tano,ambao haukuwahi kushuhudiwa katika serikali za awamu zilizopita unaipa imani kubwa ya kukubalika zaidi ya vyama vingine.
Vyama vingine haviwezi kuwa na ujasiri kama huo wa serikali ya awamu ya tano kwa kuwa viongozi wao walio wengi ni washirika wa wabadhirifu wa mali za umma.Watakachoweza kukifanya hata kama wakipewa nafasi ya kutawala kwa bahati mbaya ni kupora mali za umma badala  ya kujali maslahi ya umma.